Chama Cha Mapinduzi chajipanga kurejesha
imani kwa wananchi
Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam jana kimefanya mkutano mkubwa katika
viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam kwa nia ya kuipongeza Sekretarieti
mpya ya Chama hicho. Mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama wake kutoka Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni waliofika
kwa wingi walivifanya viwanja hivyo vya Mnazi Mmoja kulipuka kwa shangwe ya
vigelegele, ngoma na nyimbo mbali mbali.
Waliopongezwa kupitia mkutano huo ni Rais Jakaya Kikwete
aliyechaguliwa tena kushika nafasi ya Uenyekiti wa Chama kitaifa na Philip
Mangula akiwa Makamu Mwenyekiti Bara. Dk Ali Mohamed Shein Makamu Mwenyekiti
Zanzibar. Wengine ni Abdulhaman Kinana alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu na Mwigulu
Nchemba Naibu Katibu Mkuu Bara, wakati Nape Nnauye alichaguliwa kuendelea na
nafasi yake ya Katibu Mwenezi wa Chama.
Rais Kikwete alisema Sekretarieti Mpya kwa kushirikiana na
wana CCM wote nchini wana wajibu wa kurejesha imani ya watanzania kwa Chama
hicho. Alisema kuwa huu ni wakati wa kufanya tathmini ya kutosha na kuchukua
maamuzi ya kuhakikisha kuwa wananchi wanakiunga mkono CCM kama ilivyokuwa
zamani.
“Tunapaswa kufanya tathmini ni kujua nini Chama chetu
kimefanya mpaka kimekuwa na sura hiyo iliyokuwa nayo sasa kwa jamii. Tutafute
sababu ili kuwafanya wananchi waweze kukiunga mkono tena,” alisema Rais
Kikwete.
Pia ameitaka Sekretarieti hiyo kufanya mikutano ya hadhara
na mikutano ya ndani kama mkakati wa kujijenga upya. Aliwataka kuzunguka nchi
nzima na kuzungumza na wanachama na wananchi ili kurejesha tena imani ya
wananchi kwa CCM.
Naye Makamu Mwenyekiti, Philipo Mangula alisema kuwa yeye
kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chama hicho atahakikisha ndani ya miezi
sita wala rushwa na watoa rushwa watashughulikiwa vyema ili kukisafisha Chama.
Alisema wote ambao wamepata uongozi kwa njia ya rushwa hawataachwa salama na
hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Tutashughulikia malalamiko yote ndani ya miezi sita. Wote
walioingia madarakani kihalali hao
wataendelea lakini wale waliotumia rushwa hatutasubiri polisi au Takukuru, hao
hawataendelea ni lazima tuwatoe nje ya uongozi. Mlima nyanya kurudi kazini basi
juje ipo kazi,” alisisitiza Mangula.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Abdulahaman
Kinana alisema kuwa majukumu waliyonayo ni kuisimamia Serikali. Alisema Chama
hakiwezi kutimiza wajibu huo ikiwa kuna rushwa, upendeleo na mizengwe. “Kuna
tatizo la mmomonyoko wa maadili ndani ya Chama. Hatuwezi kusimamia uadilifu
kama sisi wenyewe siyo waadilifu. Tutasimamia katiba yetu, kanuni na
maelekezo ya vikao vizuri,” alisema
Kinana.
Alisisitiza kuwa uongozi ndani ya Chama siyo ajira ila ni
kujitolea. Alisema kuwa kukijenga Chama ili kukirudishia heshima kama
ilivyokuwa awali.
No comments:
Post a Comment