Monday, November 19, 2012

CCM WAPONGEZANA


Chama Cha Mapinduzi chajipanga kurejesha imani kwa wananchi

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam jana kimefanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam kwa nia ya kuipongeza Sekretarieti mpya ya Chama hicho. Mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama wake kutoka  Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni waliofika kwa wingi walivifanya viwanja hivyo vya Mnazi Mmoja kulipuka kwa shangwe ya vigelegele, ngoma na nyimbo mbali mbali.
Waliopongezwa kupitia mkutano huo ni Rais Jakaya Kikwete aliyechaguliwa tena kushika nafasi ya Uenyekiti wa Chama kitaifa na Philip Mangula akiwa Makamu Mwenyekiti Bara. Dk Ali Mohamed Shein Makamu Mwenyekiti Zanzibar. Wengine ni Abdulhaman Kinana alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu na Mwigulu Nchemba Naibu Katibu Mkuu Bara, wakati Nape Nnauye alichaguliwa kuendelea na nafasi yake ya Katibu Mwenezi wa Chama. 
Rais Kikwete alisema Sekretarieti Mpya kwa kushirikiana na wana CCM wote nchini wana wajibu wa kurejesha imani ya watanzania kwa Chama hicho. Alisema kuwa huu ni wakati wa kufanya tathmini ya kutosha na kuchukua maamuzi ya kuhakikisha kuwa wananchi wanakiunga mkono CCM kama ilivyokuwa zamani.
“Tunapaswa kufanya tathmini ni kujua nini Chama chetu kimefanya mpaka kimekuwa na sura hiyo iliyokuwa nayo sasa kwa jamii. Tutafute sababu ili kuwafanya wananchi waweze kukiunga mkono tena,” alisema Rais Kikwete.
Pia ameitaka Sekretarieti hiyo kufanya mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani kama mkakati wa kujijenga upya. Aliwataka kuzunguka nchi nzima na kuzungumza na wanachama na wananchi ili kurejesha tena imani ya wananchi kwa CCM.
Naye Makamu Mwenyekiti, Philipo Mangula alisema kuwa yeye kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chama hicho atahakikisha ndani ya miezi sita wala rushwa na watoa rushwa watashughulikiwa vyema ili kukisafisha Chama. Alisema wote ambao wamepata uongozi kwa njia ya rushwa hawataachwa salama na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Tutashughulikia malalamiko yote ndani ya miezi sita. Wote walioingia madarakani kihalali  hao wataendelea lakini wale waliotumia rushwa hatutasubiri polisi au Takukuru, hao hawataendelea ni lazima tuwatoe nje ya uongozi. Mlima nyanya kurudi kazini basi juje ipo kazi,” alisisitiza Mangula.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Abdulahaman Kinana alisema kuwa majukumu waliyonayo ni kuisimamia Serikali. Alisema Chama hakiwezi kutimiza wajibu huo ikiwa kuna rushwa, upendeleo na mizengwe. “Kuna tatizo la mmomonyoko wa maadili ndani ya Chama. Hatuwezi kusimamia uadilifu kama sisi wenyewe siyo waadilifu. Tutasimamia katiba yetu, kanuni na maelekezo  ya vikao vizuri,” alisema Kinana.
Alisisitiza kuwa uongozi ndani ya Chama siyo ajira ila ni kujitolea. Alisema kuwa kukijenga Chama ili kukirudishia heshima kama ilivyokuwa awali.

No comments:

Post a Comment